WASIFU WAKE
KUZALIWA:
Padre John Felician Mahundi alizaliwa tarehe 12/11/1958 Pongwe, Wilaya ya Tanga, Mkoa wa Tanga. Alipata Sakramenti za Ubatizo, Komunyo na
Kipaimara katika kigango cha Pongwe Mianzini, Parokia ya Mt. Anthony Chumbageni na Mt. Teresia Jimbo katoliki la Tanga.
ELIMU:
Padre Mahundi alipata elimu ya Msingi katika shule ya Msingi Pongwe na Sekondari katika Seminari ya Mt. Yosefu Soni Lushoto.
Baadaye alijiunga na Seminari kuu ya Ntungamo Bukoba na baadaye Seminari kuu ya Peramiho Songea.
DARAJA LA USHEMASI NA UPADRE:
Mwaka 1985 Padre Mahundi alipewa daraja takatifu la Ushemasi na Mwaka 1986 daraja Takatifu la Upadre katika Kanisa kuu la
Mt. Anthony wa Padua, Jimbo katoliki Tanga na Mhashamu Maurus Komba, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga.
SEHEMU ALIZOWAHI KUISHI NA KUFANYA KAZI KATIKA MAISHA YAKE.
Marehemu padre Mahundi aliwahi kufanya kazi katika sehemu mbalimbali. Baada ya Upadre wake alitumwa kufanya kazi na nyadhifa mbalimbali
kama msaidizi na Paroko katika Parokia zifuatazo:- Maramba, Mlingano, Usagara, Kanisa Kuu la Mt. Anthony wa Padua Tanga, Malindi, Kilole,
Magoma, Potwe na pia aliishi Uaskofuni.
Tarehe 20/07/2007 kwa mika 10 Padre Mahundi alifanya utume wa uchungaji Jimboni Mbeya katika Parokia ya Mt. Stefano, Mbalizi Mbeya.
UGONJWA NA MAUTI:
Padre John Felician Mahundi, kwa taarifa tulizopata, siku ya Jumapili tarehe 26/03/2017 alitoka kwenye ibada ya Misa Takatifu aliporudi
akaingia chumbani apumzike. Wakati wa chakula wenzake walimsubiri hawakumuona, walipomgongea hakuitika ndipo Paroko akafungua mlango wake na
kumkuta anakoroma. Wakamchukua kumpeleka hospitali lakini umauti ulimkuta njiani. Tarehe 27/03/2017 Mhashamu Baba Askofu Anthony M. Banzi wa
jimbo katoliki la Tanga alijulishwa juu ya msiba huu mkubwa wa mpendwa wetu Padre John Mahundi. Apumzike kwa Amani.
SHUKRANI:
Mhashamu Baba Askofu Anthony Banzi wa jimbo katoliki Tanga, pamoja na Mapadre wa jimbo la Tanga, tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati
kwa wale wote walioshiriki katika jitihada za kusaidia kuokoa maisha ya mpendwa wetu Padre John Felician Mahundi.
1. Tunapenda kutoa shukrani kwa Madaktari na Wauguzi waliomhudumia na kumuandaa kwa Moyo wa upendo Padre wetu huyu mpendwa.
2. Shukrani zetu ziwafikie pia ndugu wote wa Marehemu Padre John Felician Mahundi, kwa namna ya pekee tunamshukuru kaka wa marehemu
Christian Felician Mahundi pamoja na mtoto wake Felician Christian Mahundi walioandamana na msafara wa Mhashamu Baba Askofu kwenda kumchukua
mpendwa wetu huko Mbeya na kumleta Tanga.
3. Tunamshukuru sana kwa namna ya pekee Mhashamu Baba Askofu Evarist Chengula Sakofu wa Jimbo Katolki la Mbeya aliyempokea na kukaa naye
na kumhudumia kiroho na kimwili kwa karibu miaka kumi.
4. Tunawashukuru sana pamoja nasi Mapadre:- Pd. Renatus Mwakanyamale (PP), Pd. Elias Kingamkono (Katibu Umawata Jimbo, Pd. Venance Mbilinyi,
Pd. Gilbert Sanga, Pd. Paul Mwashiriri na Pd. Simon Msompa, Watawa:- Sr. Josephine Mbawala, Sr. Emiliana Mvovora na Sr. Judith Mwawera na Walei
21 wa Jimbo Katoliki la Mbeya pmoja na Wanaparokia wa Parokia ya Mt. Stefano Mbalizi, ambao walikaa naye kwa karibu miaka kumi katika Jimbo na
Parokia hiyo.
5. Tunawashukuru sana uongozi wa Parokia ya Kilole, Baba Paroko Pd. John Sabuni, Msaidizi wake Pd. Agustino Temu, Masista, Viongozi H/W
Parokia, Wanakwaya na waamini wote wa Parokia ya Kilole daima kwa moyo wa utayari.
6. Kwenu Waombelezaji wote mliofika hapa leo hii katika kumsindikiza na kumuaga mpendwa wetu Padre John Mahundi, nanyi pia mliojitoa
kuiandaa nyumba yake anamolazwa Mpendwa wetu, ninyi waandaaji wa mashada na waweka mishumaa nyote mpokee shukrani kwa moyo wenu huo wa kujitoa.
7. Tunawashukuru Radio Huruma, Idara ya Habari Jimbo Katoliki la Tanga, Radio One na TBC Bango kwa kutupatia taarifa hizi za msiba huu.
8. Tunakushuru sana mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Mama Yetu wa Usambara COLU - Kwamndolwa, pamoja na uongozi wake, kwa utayari wa
kushiriki katika msiba huu na michango yenu ya hali na mali ili kufanikisha shughuli zote za mazishi ya mpendwa wetu.
9. Tunawashukuru viongozi wa Halmashauri ya Walei Jimbo, Mkurugenzi wa Utume wa Walei Jimbo la Tanga, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei
Jimbo la Tanga, Viongozi mbalimbali wa Parokia za Mt. Peter Saruji, Mt. Theresia, Mt. Anthony wa Padua, Mt. Mathias Mulumba, shirikisho la
Kwaya Tanga na wote mliojitoa kwa namna ya pekee kumsindikiza katika safari yake ya mwisho Mpendwa wetu.
10. Tunatoa shukrani kwa taasisi mbalimbali, viongozi mbalimbali wakiwemo wa kisiasa na kidini tukitambua pia uwepo wako Mheshimiwa Davis
Mwamunyange, Mstaafu Mkuu wa Majeshi, Shemeji wa Marehemu, nanyi nyote ndugu, jamaa na marafiki tunatambua uwepo wenu, asanteni sana.
Imeandaliwa na kusomwa na:-
Padre Thomas J. Kiangio- Katibu Mkuu- jimbo katoliki la Tanga
Raha ya milele umpe ee Bwana, na Mwanga wa milele umuangazie, apumzike kwa amani. Amina.
catholic diocese of Tanga © 2024
|